Mabadiliko ya Tabia

UTUME KWA VIJANA 4

Sahaya G. Selvam, SDB

 

Namna ya Kuwafundishia Vijana ili

Kuleta Mabadiliko ya Tabia

 

“Semina, semina, semina! Nimechoka na semina hizi!”, kijana mmoja alinilalamikia mara baada ya kurudi kutoka Kongamano la Pasaka.

Nilikuwa ninaongea na Askofu wa jimbo moja la Tanzania, na nikamwambia, “Baba askofu, nimesikia kwamba asilimia kubwa ya vijana wa mkoa huu wameathirika na ukimwi, kama kanisa tumefanya nini kukabiliana na hali hii?”  Akanijibu mara moja kwa uhakika, “Tumefanya semina nyingi tu!”

Semina, semina, semina! Je, semina hizi huleta mabadiliko ya tabia? Au semina hizi ni njia mojawapo ya kula misaada tunayoipata kutoka nchi za nje badala ya kukabiliana na matatizo ya kijamii kama ukimwi?

Hakika, zipo njia nyingi tu za kutoa malezi kwa vijana, baadhi zake nimekwisha kuzitaja katika toleo lililopita.  Licha ya michezo na vitendo mbalimbali katika vikundi, njia kubwa ya kutoa malezi kwa vijana ni kwa njia ya mafundisho darasani, semina na warsha.  Katika makala hii, ningependa kuangalia namna gani tunaweza kuboresha semina na warsha zetu katika kuwafundisha vijana ili kuleta mabadiliko ya tabia.

 

Mabadiliko ya Tabia huletwa na Ujuzi, Stadi na Malengo

 

Kwa mfano, kama mimi ninataka kuwa mchezaji hodari wa mpira wa miguu, nitahitaji mambo matatu:

Ujuzi (Knowledge) – kujua sheria za mchezo, mfumo wa timu, n.k. Ninaweza kujifunza ujuzi wa mchezo darasani. Ingawa ujuzi ni muhimu, hata nikijua sheria zote pamoja na historia ya mchezo wenyewe, hamaanishi kuwa tayari nitakuwa mchezaji hodari.  Pamoja na ujuzi nahitaji vilevile stadi na mbinu, yaani namna ya kucheza.

Stadi (Skills) – kujifunza namna ya kupokea na kutoa pasi, namna ya kupiga chenga, namna ya kutumia viungo vya mwili katika kuchezea mpira, n.k.  Naweza kujifunza stadi kwa njia ya kufanya mazoezi uwanjani peke yake.  Siwezi kujifunza stadi darasani.

Malengo (Motivation)  – kujua moyoni mwangu kwa nini niwe mchezaji hodari.  Nikiwa na malengo makubwa, kama vile kujiunga na timu za ulaya, nitaongeza bidii katika kujenga stadi za mchezo. Hatimaye nitakuwa na mafanikio makubwa.

Vilevile kijana, katika kujifunza namna ya kuwa mkristu hodari, anahitaji ujuzi, stadi na malengo.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kijana labda anaelewa kwa akili yake anatakiwa kuwa na msimamo wa kikristu, labda anajua pia maana ya msimamo wa kikristu.  Lakini anapojikuta katika mazingira magumu anashindwa kwa sababu labda hana stadi za maisha ya kikristu, na labda hajui kwa nini anapaswa awe mtu mzuri.

Upungufu wa semina zetu mara nyingi ni kwamba, katika semina tunawapa ujuzi tu! Tunawaambia vijana, “uwe mtu mzuri; sema ‘hapana’ kwa mapenzi kabla ya ndoa; usitumie kondomu, n.k.”  Katika semina hizi vijana huwa wanaandika muhtasari kwa kirefu, wanarudi katika mazingira yao.  Kumbe, hakuna mabadiliko ya tabia!  Tatizo ni kwamba mara nyingi hatuwafundishii stadi za maisha – namna ya kujifahamu, kujithamini, namna ya kujenga uhusiano mzuri na watu, mbinu za uamuzi, mbinu za kutatua matatizo, namna ya kukabiliana na shinikizo za mazingira, n.k.

 

 

Stadi za Maisha hujengwa na mbinu shirikishi

 

Vijana daima wanapenda sana kuwa katika hali ya uchangamfu.  Wanaweza kujifunza hata mambo magumu na mazito wakiwa wamechangamka.  Vijana wanapocheza na  kujadiliana wanajifunza bila kuona ugumu wa darasani.  Mbinu ya mhadhara (Lecture Method) ni mbinu hafifu hasa vijana wanapojifunza mambo ya kijamii na kidini.

Vijana wenyewe wanafahamu mambo mengi.  Wakipewa nafasi, wapo tayari kushirikiana na wenzao kujadiliana juu ya yale wanayoyafahamu.  Wanaposhirikiana hivyo, wanaweza kuufikia uamuzi wa kuyatimiza katika maisha yao, bila msukumo wowote.  Katika hali hiyo kazi ya mlezi ni kuwatengenezea mazingira ya kuutambua, kuushirikisha na kuuimarisha msimamo wao.  Mlezi huwa anahakikisha kwamba msimamo wao ni kweli na halali.

Hapa chini ningependa kuoredhesha mbinu chache za kujenga stadi na malengo kati ya vijana.

 

 

Mbinu Bunifu za Kuwafundishia Vijana

  1. Zoezi la kuafiki ama kutoafikiana.

Hii ni sentensi kadhaa juu ya mada fulani. Kila mshiriki huonesha kama anakubaliana au hakubaliani na sentensi hizo, kwa njia ya kutoa maoni yake.  Faida yake ni kwamba huamsha na kuwezesha ufikiriaji.

  1. Bunga Bongo (Brain-Storming)

Washiriki huchangia mawazo mengi kadiri iwezekanavyo juu ya mada iliyotolewa. Mawazo hayo hayachambuliwi wala kukataliwa mwanzoni.  Yanaweza kuorodheshwa ubaoni au kwenye karatasi ya kielelezo.  Lakini wakishamaliza kuchangia, uchambuzi huanza.

  1. Majadiliano ya vikundi.

Majadiliano hufanyika katika vikundi vidogo vidogo vya washiriki kati ya wanne na wanane. Vikundi vidogo huwapa vijana nafasi kushirikisha mawazo bila hofu.

  1. Masimulizi

Masimulizi ni kutumia hadithi au kisa katika kueleza mada fulani. Husaidia kuwaingiza vijana katika mada, na kuwagusa moyoni.

  1. Kisa Mkasa (Case Study)

Hali halisi ya maisha huwasilishwa kutokana na hadithi zinazotoka magazetini. Mifano hii isimuliwe kama matukio ya kweli.  Vikundi vichunguze na kupendekeza suluhisho. Mbinu hii husaidia ufikiriaji na uchambuzi.

  1. Uchoraji bunifu.

Washiriki hutoa michoro inayowakilisha mawazo na hisia zao. Kisha hushirikishana michoro hiyo katika vikundi vyao. Mbinu hii huongeza ubunifu na kudhihirisha hisia na mawazo.

  1. Uandishi bunifu.

Matumizi ya mashairi, insha, tamthilia ili kuelezea kina cha tatizo kwa maandishi.

 

  1. Tamthilia.

Kuonesha hali fulani kwa mchezo wa igizo lililoandaliwa. Tamthilia huonesha hata jambo zito kwa njia ya kichekesho.

  1. Mdahalo (Debate)

Timu mbili zinarumbana juu ya mada.  Kusikia pande zote mbili kunasaidia kuelewa kina cha tatizo.

10.  Hija.

Kutembelea sehemu ya makumbusho, kanisa, au vituo fulani. Ni nafasi ya kufanya toba, kusali, kufanya matendo ya huruma, na kujifunza elimu ya kidini.

11.  Lugha ya picha (Photo-language)

Kutoka katika mkusanyiko wa picha, kila mtu huchagua picha moja kuwakilisha mada fulani. Kisha hufuatiliwa na kushirikishana katika vikundi. Picha hizi zinauzwa kama vielelezo vya katekesi au zinaweza kukusanywa kutoka magazeti ya zamani.  Mwalimu anaweza kutumia pia picha hizo katika simulizi ya hadithi.

12.  Filamu na video.

Maonesho ya picha na filamu zenye mada yafaayo kwa ufafanuzi. Majadiliano yanaweza kufuata. Husaidia usikivu, ushirikiano na kumbukumbu. Lakini mlezi awe makini katika kuchagua filamu inayofaa umri wa washiriki.

13.  Igizo Dhima (Role Play)

Hali halisi ya maisha huwekwa katika mtindo wa michezo ya igizo. Mbinu hii ni  tofauti na tamthilia kwa vile michezo hii inaandaliwa palepale darasani. Ni mbinu nzuri katika kufundisha stadi za maisha.  Kwa mfano vijana wanapoonesha namna ya kuwasiliana na wazazi, mlezi ana nafasi

 

14.  Mahojiano (Interview).

Kumhoji mgeni-mtalaamu juu ya mada fulani.  Mwalimu mwenyewe anaweza kuhoji mwalikwa au mmojawapo wa wanafunzi.  Halafu kujadili pamoja majibu yake.

 

15.  Uchunguzi wa magazeti.

Kuchambua magazeti ili kupata habari juu ya mada fulani. Huhamasisha vitendo, hivyo husababisha kujifunza.

 

16.  Jopo (Paneli)

Majadiliano yafanywayo na wataalamu kadhaa. Wanafunzi wanapata nafasi ya kuwahoji pia.

17.  Muziki.

Kundi husikiliza muziki ya kisasa na kujadili mada mbalimbali au hisia kutokana na muziki ule. Muziki ilichaguliwa vizuri inachochea majadiliano mazuri.

18.  Adhimisho la Liturjia

Adhimisho la ibada hasa ya Ekaristi takatifu ni nafasi ya kuunganika na Mungu.  Licha ya hiyo, ibada ni nafasi ya katekesi.  Maadhimisho yaliyoandaliwa vizuri yanaweza kuwafundisha vijana maana ya imani yetu.

19.  Mazoezi ya Kiroho

Mazoezi ya kiroho si tunu zilizotolewa kwa mapadre na watawa tu, bali ni mali ya wakristu wote.  Mazoezi ya kiroho kama sala, mfungo (recollection & retreat), hata semina ni nafasi nzuri ya kufundisha dini.

 

20.  Sherehe za Sikukuu

Sherehe huwafurahisha vijana.  Aidha, zinaweza kuwafundisha.  Sikukuu za watakatifu, sikukuu za adhimisho la sakramenti kama ubatizo, komunyo ya kwanza, kipaimara, ndoa, upadrisho na hata ya mpako wa wagonjwa zinaelimisha washiriki, ikiwa zimeandaliwa vizuri, pamoja na mafundisho na ibada.

 

 

Hitimisho

 

Katika utume wowote hasa kwa vijana, mlezi hana budi kuelewa kwamba tusipoona mabadiliko ya tabia kati ya walengwa hatuna sababu ya kukata tamaa.  Ndiyo, tusipopata mafanikio tunalazimika kutathmini mbinu zetu. Lakini mafanikio ya utume mara nyingi hayapimiki mara moja; tena mageuzi ya mioyo ni kazi ya Roho Mtakatifu.  Pamoja na kujitolea kwake mlezi, vinavyoleta mabadiliko ya mtu ni uaamuzi wa mtu mwenyewe pamoja na neema ya Mungu.  Mlezi hupeleka kijana kwenye maji, kunywa maji yale ni juu ya kijana mwenyewe.  Mlezi huonesha njia, kutembea katika njia ile ni juu ya uaamuzi wa kijana mwenyewe. Wajibu wa mlezi ni kuandaa uwanja na kupanda mbegu, kwa ushirikiano wa mtu binafsi Mungu ndiye anayefanikisha mazao.

 

(Itaendelea…)