Katekisimu kwa ajili ya Vijana – 1

UTUME KWA VIJANA – 16

Sahaya G. Selvam, SDB

Katekisimu kwa ajili ya Vijana – 1

Utangulizi:

Kutokana na uzoefu wangu wa kutoa semina na mafungo kwa ajili ya vijana katika nchi za Afrika Mashariki nimeona kuwa vijana wengi wana maoni kuhusu imani ya kikristu ambayo ni hafifu.  Wengine wana msimamo wa kikristu ambao unawabana mno, hata wanaona hawawezi kuwa wakristu wakamilifu.  Wengi wanaishi na mgogoro kati ya imani iliyo kali na maadili ya kujiruhusu mno. Kutokana na katekesi potofu vijana wengi wana msimamo wa zamani, au msimamo ambao hauendani na mafundisho rasmi ya kanisa la sasa.  Kwa ujumla, uelewa wa imani yao haujakua kadiri ya ukuaji wa umri na maendeleo ya historia ya dunia na kanisa.

Katika makala hii basi, ningependa kutoa kwa mtindo wa maswali na majibu mawazo machache yanayoweza kuleta picha ya ukristu yenye furaha na uhuru.  Yesu alisema nimekuja ili muwe na uhai, tena uhai tele (Yn 10:10).  Kwa hiyo, lengo la maisha ni kuadhimisha uhai!  Je, imani yetu ya kikristu inatusaidia kuadhimisha uhai?

Lengo la “katekisimu”  hii ni kuwasindikiza vijana kukua kiimani kulingana na ukuaji wa umri, elimu na uelewano.  Hii inafaa kwa vijana hasa wale waliomaliza shule ya sekondari (O level). Mawazo haya ni yangu binafsi, kwa hiyo bado yanaweza kuboreshwa. Na mawazo hayahusu kanuni ya imani, bali yana lengo la kuleta maana katika maisha ya kiroho.  Lakini nadhani hakuna wazo hapa lililo kinyume na fundisho rasmi la kanisa kwa ujumla.  Sehemu nyingine ya maswali na majibu haya zinaweza kuwa tofauti na yale tuliyokariri tulipokuwa tunajiandaa kwa ajili ya sakramenti za komunyo ya kwanza na kipaimara.  Kusudi la majibu haya hasa ni kuelewa kwa undani tuliyokariri hapo awali ili imani yetu ikuwe kadiri ya umri wetu.

Nimechagua maswali 25 tu, tunaweza kuendelea kuongeza mengine. Lakini nimeona kijana akielewa haya anaweza kuishi kwa undani zaidi maisha yake ya kikristu.  Maisha ya kikristu ni zaidi ya kutii amri na kutimiza wajibu wa kwenda kanisani.  Maisha ya kikristu ni hata zaidi ya kukariri katekisimu kwa lengo la kupokea sakramenti.  Maisha ya kikristu ni maisha ya ndani.  Ni mchakato wa ukuaji katika uhusiano kati ya kijana na nafsi yake mwenyewe – kujielewa na kujikubali; uhusiano wangu na Mungu – kumtambua, kuuitikia uwepo wake katika sala, na hatimaye kuunganika naye; na kujenga uhusiano na majirani zake – kuwapenda bila ubinafsi, kuukuza utu na uhai wa binadamu.

Hapa sijajibu maswali mengine yanayoulizwa na vijana, ambayo ni marudio ya maswali ya watu wa madhehebu mengine, kama, “Kwa nini tunaabudu sanamu?”  Vijana Wakatoliki wanahitaji kuhimizwa kuelewa kwa undani imani yao yenyewe badala ya kurudia maswali yanayoulizwa na watu wengine.  Maswali yako mengi tu, kama yale ya hapo juu, ambayo tunaweza kuuliza, kwa nini kurudia maswali ya wengine?  Labda ni kwa sababu sisi wenyewe hatuna uhakika na imani yetu.  Basi lengo mojawapo la makala hii ni pia kuchochea maswali yenye maana na ya kina zaidi ili tuelewe kwa undani zaidi imani yetu.


1. Kiini cha Ukristu ni nini?

Ni Mungu katika nafsi ya Yesu Kristu.

Kuna uwezekano wa kuwa na majibu tofauti ambayo ni hafifu kwa sababu zifuatazo:  k.m. Imani – imani ya kikristu si kanuni wala falsafa bali ni nafsi, yaani nafsi ya Yesu Kristu.  Upendo- Ingawa upendo una umuhimu wake katika Ukristu,  ni matokeo tu  ya kumjua Yesu.

 

2. Lengo kuu la Ukristu ni nini?

Kuambatana na Yesu Kristu.

Kuwa mkristu haitoshi kujua historia ya Yesu, wala kumjua Yesu kwa akili.  Bali lengo la Ukristu ni kuambatana na Yesu. (Soma Yohane 1: 35-41) Yaani, kuwa na mang’amuzi ya binafsi ya Yesu Kristu, kwa msaada wa jumuiya ya kanisa.

 

3. Namna gani naweza kuambatana na Yesu Kristu?

Kwa kifupi kwa njia ya sala.  Lakini pia sakramenti za kanisa, hasa Ekaristi; Ibada za pamoja, tafakari, lectio divina (ni mbinu ya kusali kwa kutumia Biblia), n.k., zinaweza kunisindikiza katika safari ya kumjua Yesu.

Tunajua kwamba tunasema sala nyingi, lakini mara nyingi hatusali.  Sala ambayo inaweza kutusaidia kumng’amua Yesu ni aina ya sala ya contemplatio! Yaani, kusali kwa kutumia moyo na hisia  kuliko akili zetu. Katika maisha yetu ya kikristu tunahitaji kukomaa katika sala; kuvuka kutoka sala ya maombi kwenda sala ya tafakari na contemplatio!

4. Sala ndiyo nini?

Sala ni tendo la kujenga uhusiano na Mungu.

Sala halisi inaanza na kujitambua katika uwepo wa Mungu, na huishia katika kumtambua Mungu/Yesu mwenyewe.  Hatua ya kwanza katika sala ni utambuzi – kutambua uwepo wa Mungu na upendo wake; na kujitambua mimi ni nani katika uwepo wake.  Ninapojitambua kuwa mimi ni kiumbe tu mbele ya Mungu, ninawasilisha hisia zangu katika sala ya sifa. Ninapotambua kuwa amenitendea mambo makuu ninaanza kutoa sala za shukrani.  Ninapotambua kuwa yeye ndiye ananikirimia mahitaji yangu yote ninatoa sala za maombi.  Ninapojitambua kuwa mwenye dhambi ninawakilisha hisia zangu katika sala ya msamaha. Hatua ya pili katika sala ni kumsikiliza Mungu.  Ninapomsikiliza kwa kupitia maandiko matakatifu hii ni lectio divina.  Na hatimaye ninapoanza kumtazama Mungu katika ukimya na kutambua anavyowasiliana nami katika hisia za moyo wangu hii ni sala ya contemplatio.

 

5. Biblia ina nafasi gani katika maisha ya kikristu?

Biblia ni Neno la Mungu linalohifadhiwa katika maandishi, na inatoa maelezo na ukweli kuhusu Mungu mwenye na maisha yetu ya binadamu.  Vilevile Biblia inatuelekeza namna ya kujenga uhusiano na Mungu na wenzetu kwa njia ya maadili mema.  Aidha Biblia ni chombo cha sala.

Maandiko matakatifu yaliandikwa na binadamu kwa uwezo wa Mungu.  Mungu akawafunulia na waandishi wanaandika kwa kutumia lugha za binadamu.  Ndani ya Biblia kuna mitindo mbalimbali ya matumizi ya lugha, na tunahitaji kuzingatia hilo tunapochambua ukweli wa ufunuo wa Mungu. (Rejea Mtaguso II wa Vatikano, Dei Verbum, na. 11-13) Biblia ya wakristu ina sehemu mbili kuu – Agano la Kale (AK) and Agano Jipya (AJ).  AJ linakamilisha AK. Biblia ina ukweli kuhusu hali ya Mungu, historia ya Wokovu, hali ya ubinadamu na mwongozo kuhusu maadili.  Aidha, Biblia ni hazina ya sala.

 

6. Ekaristi inaweza kunisaidia namna gani?

Ekaristi kama Ibada inanisaidia kuunganika na jumuiya ili kuambatana na Mungu katika nafsi ya Yesu Kristu; Ekaristi kama Sakramenti inanikumbushia uwepo wa Mungu katika umbo la mkate. Ekaristi kama Komunyo inanisaidia “kushiriki katika umungu wake yeye aliyekubali kushiriki katika ubinadamu wetu”, hivyo kuambatana na Mungu katika nafsi ya Yesu Kristu.

 

7. Je, ni lazima kupokea Komunyo kila ninaposhiriki katika adhimisho la Ekaristi?

Inafaa kupokea komunyo takatifu kila ninaposhiriki katika Misa Takatifu nikiwa katika hali ya neema, yaani bila dhambi ya mauti.

Adhimisho la Ekaristi takatifu ni sadaka na mlo.  Sadaka inakamilishwa katika mlo.  Ninashiriki kikamilifu katika sadaka ninaposhiriki katika chakula cha matoleo – ambacho kimekuwa mwili na damu ya Yesu.  Changamoto kwangu ni kujiweka daima katika hali ya neema (usafi wa roho) ili niweze kupokea komunyo kila ninaposhiriki katika misa takatifu.

 

8. Je, nikiwa na chuki na mwenzangu naruhusiwa kupokea Ekaristi?

Kitu kinachoweza kunizuia katika kupokea Ekaristi ni dhambi ya mauti tu.

Kweli dhambi ndogondogo zinaharibu usafi wa roho zetu. Lakini katika Ibada ya Toba katika sehemu ya kwanza ya misa (yaani, tunaposali “Nakuungamia Mungu Mwenyezi.. au Bwana Utuhurumie….”) tunaweza kukiri dhambi hizi na kujiweka tayari kuadhimisha na kushiriki katika Ekaristi.  Lakini dhambi ya mauti zinageuza mwelekeo wetu kabisa, kwa hiyo tunahitaji kuziungama ili tukidhi uponyaji wa roho. (Angalia Swali 9.)

 

9. Dhambi ndiyo nini, basi?

Tendo lolote linanohatarisha uhai na utu ni dhambi.

Tunapouhatarisha uhai na utu ulioumbwa na Mungu tunajitenga na Mungu; tunajitenga na jamii pia na hatimaye tunajijeruhi wenyewe. Hayo ndiyo matokeo ya dhambi. Dhambi zilizotendeka hata katika siri zinahatarisha utu wa walioshiriki katika tendo lile, pamoja na kuharibu utu wangu mwenyewe.

 

10. Taja vipengele vitatu vinavyochangia katika kuzidisha uzito wa dhambi?

Kwanza tendo lenyewe, pia nia na mazingira ya dhambi.

Yapo matendo mengine ambayo yana uzito wa dhambi tayari kama kwa mfano uuaji; mengine hayana uzito kama kupiga chafya!  Lakini karibu matendo mengi yanaweza kuzidisha au kupunguza uzito wa kimaadili yakitegemea na mazingira na nia ya mwenye kutenda.  Kwa mfano, kama umemwua mtu bahati mbaya katika mazingira ya mashambulizi, tena kwa lengo la kujisalimisha, tendo hili litakuwa na uzito mdogo kuliko kumwua mtu baada ya kutafakari siku nyingi na kwa mpangilio maalumu.

 

11. Dhambi ya mauti ndiyo nini?

Dhambi ya mauti kwa lugha rahisi ni dhambi kubwa ambayo mtu anatenda akiwa na utashi na ufahamu kabisa, kwa kusudi.  Kwa lugha nyingine dhambi ya mauti ni tendo ambalo linaweza kubadilisha mwekeleo wangu (fundamental option) kabisa.  Yaani, linaweza kuwa chanzo cha mazoea mabaya.