Vijana na Dini

UTUME KWA VIJANA – 15

Sahaya G. Selvam, SDB

Vijana na Dini

Ilikuwa Jumapili asubuhi.  Nilikuwa najiandaa kwenda kwenye ibada, simu yangu ya mikononi ikalia.  Kulikuwa na sms kutoka msichana mmoja ambaye aliwahi kuwa mwanafunzi wangu katika Chuo Kikuu.  Ujumbe ukasema, “Padre, sijisikii kwenda kwenye misa leo.  Nataka kwenda.  Je, unaweza kunipa sababu tatu ili kunimotisha kwenda kanisani?”  Nikampa sababu moja tu, “Yesu anakusubiri!”  Basi, hatimaye akaenda!

 

Barani Afrika kati ya washiriki wa ibada za kanisani bado wengi ni vijana.  Vyama vya vijana viko hai sehemu nyingi, na vijana wanachangia kiasi kikubwa katika kuboresha liturjia, kwa njia ya kuimba na kucheza ngoma za kiliturjia. Je, vijana kweli wanajisikia nyumbani katika kanisa?  Je, kanisa linatimizia kweli mahitaji ya vijana? Je, mambo ya dini ni kwa ajili ya wazee tu?   Na kwa nini baadhi ya vijana wamekuwa watalii wa kidini – yaani wanapenda kutembelea makanisa mengi kuonja mahubiri na liturjia tofauti tofauti?  Katika makala hii tujitahidi kujibu maswali haya, na kupendekeza mambo yatakayochangia katika kuwaridhisha vijana kiimani.

 

Mahitaji ya Kiroho

Binadamu ana vipengele vinne katika nafsi yake – mwili, akili, moyo na roho.  Kutokana na vipengele hivi vinne tunayo mahitaji manne. Hitaji la kimwili ni ile hali ya kulinda uhai wetu kwa njia ya kula, kunywa na kulala, n.k. Hitaji la kiakili ni ile hamu ya kujua mambo na kutafuta maelezo kwa matukio mbalimbali ya dunia.   Hitaji la kimoyo ni ule uwezo wa kuwapenda watu na kupendwa nao.  Hitaji la kiroho ni ile ari ya kumjua Mungu na kuambatana naye.

 

Katika utoto mahitaji haya yapo kwa kiwango tofauti na yanaridhishwa kwa msaada ya watu wazima.  Katika ujana kuna mwamko wa mahitaji haya na kijana anaanza kutafuta njia zake za binafsi kuridhisha mahitaji haya. Kutokana na mabadiliko ya kimaumbile kijana anatambua jinsia yake na ana nguvu ya ajabu ya kimwili.  Ana hamu ya kula sana, na kufanya mazoezi ya viungo vya mwili.  Kiakili pia anajitambua na anaweza kuwa na udadisi wa kupata maarifa mbalimbali. Anauliza maswali mengi kwa lengo la kupata maelezo. Kimoyo ana shauku la kujenga mahusiano na watu, hata watu wa jinsia tofauti.  Hitaji lake la kupenda na kupendwa liko juu sana.  Vilevile hitaji lake la kiroho linaongezeka.

 

Hapo mwanzo Mungu aliwaumba wanadamu kwa mfano wake.  Roho zetu ndizo zinazofanana na Mungu.  Kama Mungu ni bahari kubwa, roho zetu ni kama matone ya maji.  Kama Mungu ni moto mkubwa, roho zetu ni kama cheche za moto.  Roho ya mtu, kutokona na asili yake inataka kuambatana na Mungu aliye alfa na omega yake.  Ndiyo maana Mt. Augustino aliwahi kusema, “Roho yangu imetengenezwa kwa ajili yako, eh Bwana.   Inaendelea kuhangaika mpaka itulie katika nafsi yako.”

 

Nafasi na Wajibu wa Dini

Dini ina nafasi kubwa katika kutimiza mahitaji mbalimbali za wanadamu.  Ukristu tangu mwanzo umechangia kiasi kikubwa katika maendeleo ya watu katika kutimiza mahitaji yao ya kimwili, kiakili na kijamii.  Kanisa hata leo lina sehemu kubwa katika kutoa huduma ya afya na kufikisha chakula kwa ajili ya wenye njaa.  Tena Kanisa limechukua wajibu kukuza elimu ya kidunia.  Imani inayopendekezwa na kanisa inatoa maelezo yenye maana kwa mafumbo ya maisha ya kibinadamu: Nani ameniumba?  Kwa lengo gani nimeumbwa? Niishi namna gani maisha yangu ya kiubinadamu?  Hatima ya maisha yangu ni nini?

 

Dini inatimizia pia hitaji langu la kuwa sehemu ya jamii fulani.  Kwa njia ya ubatizo ninaingizwa rasmi kuwa mwanajumuiya.  Kutokana na hali ya kuwa sehemu ya jumuiya ninajitambua kuwa mtu.  Licha ya hayo yote dini inaonesha njia za kujiridhisha kiroho na namna ya kupata mang’amuzi ya kimungu, yaani kuambatana naye Mungu!

Mchoro huu unaonesha kuwa kama dini nyingine, ukristu pia una vipengele vitatu –

Kanuni ya maadili, Kanuni ya Imani na Mtindo wa Ibada.  Kanuni ya maadili inachangia katika kuboresha maisha ya kijamii.  Yaani, ninapofuata msimamo wa kimaadili maisha yangu ya kijamii huendelea vizuri.  Kanuni ya Imani inanipa maelezo kwa mafumbo ya maisha yangu – Mungu ni nani?  Aliniumba kwa lengo gani?  Baada ya kifo changu kutakuwa na nini? N.k.

 

Kipengele cha tatu ni ibada na mbinu za sala.  Ibada inanielekeza namna ya kujenga uhusiano wa karibu na Mungu ili nijiridhishe kiroho.  Kiu niliyo nayo rohoni kwa Mungu inatulizwa na Ukristu kwa njia ya sala na ibada, hasa katika adhimisho la Ekaristi Takatifu.

 

Vipengele hivi vitatu vinaweza kuwa na nafasi mbalimbali katika utoto, ujana na utu uzima.  Mtoto anapozaliwa katika familia ya kikristu, kwa kawaida anaingizwa katika dini ya wazazi wake kwa njia ya kumfundisha kanuni za ukristu, hasa kwa mtindo wa kukariri na kuiga.  Mtoto ingawa mwanzoni anajifunza kanuni za kimaadili, anapopata ufahamu anajifunza vipengele vya kanuni ya imani ya kikristu. Kadiri ya utaratibu wa kanisa zoezi hili linafanyika wakati wa maandalizi wa kupokea Sakramenti za kanisa.

Mtoto anapoingia katika ujana angependa kujua sababu na maelezo kwa kanuni hizi.  Mara nyingi watu wazima – wazazi na walezi wetu – wanashindwa kuwaelewa vijana; kuwapa sababu za kuwaridhisha ili wapate kuelewa kwa undani zaidi imani yao.  Katika ujana ari ile ya kuambatana na Mungu pia inaongezeka.  Kijana anatafuta njia za kutuliza kiu ya kiroho.  Anapopata nafasi ya kumng’amua Mungu anaelewa maana ya maisha yake na kuelewa umuhimu wa kanuni katika maisha yake.  Hivyo katika utu uzima anaendelea kuwafundishia watoto wake kanuni hizi.  Hii ndiyo ziara ya maisha ya binadamu kulingana na dini.

 

Vijana na Kanisa

 

Kama asilimia 75 ya idadi ya watu katika nchi za Afrika Mashariki ni watu wenye umri chini ya miaka 30, basi Kanisa Katoliki linahitaji kuwa na nafasi ya pekee kwa ajili ya watoto na vijana.  Kama tulivyoeleza hapo juu vijana hutazamia kupata maelezo kwa imani yao na kusindikizwa kupata nafasi ya kuambatana na Mungu.  Lakini katekesi ambayo hailingani na umri wa vijana, na ibada ambayo haina ladha ya mang’amuzi ya kimungu inawachosha.  Na hatimaye vijana wanaweza kukata tamaa na kanisa.  Wengine wanaendelea kutafuta namna ya kutuliza kiu yao katika muziki, disko, madawa ya kulevya na hata katika ngono.  Wengine kati yao wamekuwa watalii wa dini wakiyatembelea makanisa yanayoonekana kuwapa nafasi ya kuridhisha kiu yao.

Kwa hiyo, katika Kanisa Katoliki namna gani tunaweza kuwalisha vijana wetu kiakili na kiroho?  Ningependa kupendekeza vipengele vichache vinavyoweza kuwasaidia vijana ili kuwasindikiza katika safari yao ya kumtafuta Mungu:

 

1. Katekesi Endelevu:

Katika Kanisa Katoliki mara nyingi vijana waliomaliza kupokea sakramenti ya Kipaimara wanaachwa bila katekesi maalumu.  Wanapohitaji msaada wa kiroho kwa namna ya pekee inaonekana kuwa kanisa haliwajali vijana.  Ingawa hatuwezi kuwafundisha vijana wakubwa kama tunavyofundisha watoto, katekesi yenyewe inahitaji kuendelea.  Labda wanahitaji kufundishwa katika mazingira ya shule, labda kwa njia ya mfumo wa vyama vya vijana wanaweza kupatiwa nafasi ya kuelewa imani yao kwa undani zaidi.  Vilevile liturjia iliyoandaliwa vizuri inaweza kuwavutia vijana kutambua kiu yao ya kiroho.  Semina za mara moja kwa mwaka labda haitasaidia sana.  Lakini semina endelevu pamoja na mafungo ya kiroho yanaweza kuwasaidia sana.

Katika parokia moja jijini Nairobi nimewahi kuona mpangilio mzuri wa Katekesi endelevu kwa ajili ya vijana.  Kila Jumapili ya mwisho ya mwezi vijana wote wanakusanyika katika ukumbi wa parokia, ratiba ya siku ni kama ifuatavyo:

 

Saa 2.30 asubuhi – Kuwasili na kusajiliwa
Saa 3.00 – Ibada fupi ya sala ya asubuhi kwa kutumia mtindo wa Taize’ au mtindo wa Sala ya Kanisa – yaani Masifu ya Asubuhi, au “Praise and Worship”.
Saa 3.45 – Mafundisho yanayotolewa na padre mgeni kadiri ya mfululizo ya mada ya mwaka mzima. Padre anaombwa kutumia mbinu shirikishi katika kuwakilisha mada.  Mada yenyewe inaweza kulingana na dhamira ya ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa vijana katika Sikukuu ya Vijana Duniani.
Saa 4.45 – Mapumziko
Saa 5.00 – Majadiliano katika vikundi na kuhitimisha mada
Saa 5.45 – Mapumziko na maandalizi kwa ajili ya misa
Saa 6.00 – Misa takatifu – Misa yenyewe ni kwa mtindi shirikishi.  Sehemu mbalimbali zinaandaliwa na vyama mbalimbali vya vijana parokiani.
Saa 7.30 – Chakula – kwa bei nafuu.  Kila kijana ananunua chakula kutoka akina mama waliowapikia kwa msaada wa Parokia.
Saa 8.30 – Michezo iliyoandaliwa na vikundi vya vijana juu ya mada ya siku ile.
Saa 10.00 – Matangazo hasa juu ya siku ya katekesi itakayofuata, kutathmini ratiba ya siku yenyewe, na sala fupi.  Kuagana.

 

2. Vyama vya Vijana vyenye malengo na ratiba maalumu:

Licha ya kuwa na matukio maalumu kama yaliyoelezwa hapo juu, katekesi endelevu hufanyika katika vyama vya vijana. Tumewahi kueleza nafasi ya vyama katika malezi endelevu ya vijana.  Kutumia vyama vya kiutume kwa ajili ya malezi ya vijana kwanza tunahitaji kuwa na mfumo mzuri wa vyama.  Halafu tunahitaji kuwapa vijana programu zenye mpangilio.  Programu hizi zinaweza kuhakikisha malezi endelevu ya vijana.  Vyama bila programu ni kama kuwa na majengo bila matumizi.  Kama vyama hivi vya vijana havina mpangilio maalumu, vijana huwa wanaanza kuzungumza kuhusu mchango na mradi bila malengo maalumu, na hatimaye vyama vinasambaratika.

 

3. Liturjia Shirikishi:

Liturjia ni nafasi ya pekee ya katekesi katika maisha ya kikristu.  Lakini kufanikisha katekesi, liturjia iwe imeandaliwa vizuri na tena inatoa nafasi kwa wote kushiriki.  Vijana wanapenda mambo mapya.  Kwa hiyo wanaoandaa liturjia ya vijana wanahitaji ubunifu wa hali ya juu bila kuvuruga utaratibu wa liturjia.  Tena vijana hawapendi kuwa watazamaji tu katika liturjia, kwa hiyo liturjia iwe kwa mtindo shirikishi.  Hatimaye waongozaji wa liturjia wasisahau kuwa lengo kuu la liturjia ni kuwasaidia watu, hasa vijana, kuambatana na Mungu.  Yaani, kuridhisha kiu ya kiroho.

Kama ukristu unatakiwa kutimiza wajibu wake wa wokovu katika dunia hii, ukristu unahitaji waandamizi na wafuasi.  Wafuasi hodari wa ukristu wataongezeka kutoka kati ya vizazi vipya.  Na kupata vizazi vipya tunahitaji kulenga watoto na vijana wa leo.  Tayari walau mambo kadhaa yanafanika katika kanisa kwa ajili ya watoto kwa ajili ya maandalizi ya sakramenti.  Sasa tunahitaji kuongeza jitihada kuwavutia vijana ili wawe wafuasi hodari katika kanisa.  Lakini watakuwa wafuasi hodari endapo tu kiu yao ya kiroho itaridhishwa.